Aliyechomwa mkuki mdomoni asimulia


MKAZI wa kitongoji cha Upangwani, Kijiji cha Dodoma Isanga, Kata ya Masanze, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Augustino Mtitu, aliyechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni, amemshukuru Mungu, madaktari, uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa na wananchi wa kijiji hicho kwa kuwezesha kunusuru maisha yake.

Mkuki huo ulimjeruhi na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kufanyiwa upasuaji na kufanikiwa kuondolewa mkuki huo na kuokoa maisha yake.

Mtitu (42) ambaye ni mkulima alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi akiwa wodi namba moja, inayolaza wagonjwa wa majeraha ya ajali katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro.

Mkulima huyo na wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu zilizohusisha jamii ya wafugaji wa kimasai na wakulima wa kijiji hicho kilichopo katika wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.

Tukio hilo lililotokea saa 5:00 asubuhi Desemba 25 mwaka huu.

Alisema licha ya sasa kuendelea vizuri, alipata maumivu makali kuanzia muda wa kuchomwa mkuki huo na kulazimika kuushikilia mkononi mkuki kuanzia muda huo hadi saa 10:00 jioni ya siku hiyo alipofikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na madaktari kumfanyia upasuaji na kuutoa.

“Namshukuru Mungu, pia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Frank Jacob waliofika kuniona na kunifariji na leo (jana) amenitembelea Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule na baadhi ya ndugu zangu wa kijijini Dodoma Isanga,” alisema.

Hata hivyo, hakuweza kuzungumza mwa muda mrefu kutokana na sehemu ya jeraha bado ikiletea maumivu, ingawa alisema si kama yaliyokuwa siku ya kwanza baada ya upasuaji.

Katika wodi hiyo, wananchi waliokuwa wakienda kuwaanglia ndugu zao waliolazwa walikuwa wakimiminika eneo la kitanda chake wakimjulia hali na kumpa pole kwa mkasa huo wa aina yake.

Naye Stanley Andrea, ndugu wa Mtitu, ambaye yupo katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro akimuunguza nduguye, alisema hali yake inaleta matumaini ya kupona na kwamba kwa sasa anaweza kula vyakula laini.

IMEANDIKWA NA JOHN NDITI-habarileo MOROGORO

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.