PETER SERUKAMBA AKWEPA KUSALIMIANA NA MH. LOWASA

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, jana alikwepa kusalimiana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa mjini Dodoma. 

Lowassa ambaye alikuwa ameandamana na Waziri Mkuu mstaafu, Fredereck Sumaye na viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana walitembelea bungeni kwa mwaliko wa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe. 

Vigogo hao ambao walitambulishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga waliamsha shangwe kwa wabunge wa kambi ya upinzani, huku wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwa wamekaa kimya na wengine wakitabasamu. 

Baada ya Bunge kuahirishwa mchana, viongozi hao walitoka nje na kusalimiwa na wabunge mbalimbali, akiwemo Mbunge wa Newala, George Mkuchika, Mussa Ntimizi (Igalula), Venance Mwamoto (Kilolo) ambao wote wanatoka CCM. 

Serukamba ni moja ya vijana watiifu kwa Lowassa, ambaye kwa miaka kadhaa, alikuwa akimuunga mkono na wakati wote wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM katika kinyang’anyiro cha kuwania urais mwaka 2015 alikua mstari wa mbele. 

Taarifa zilizojiri katika mitandao ya kijamii zinaeleza kuwa, sababu iliyomfanya Serukamba amkimbie Lowassa ni kuogopa taarifa kumfikia Rais Dk. John Magufuli, ambapo wanaCCM waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa ndani ya chama hicho hawaaminiki katika Serikali ya awamu ya tano. 

Katika msafara huo, Lowassa na Sumaye walikuwa wameandamana na wajumbe wenzao wa Kamati Kuu ya Chadema ambao ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Profesa Abdallah Safari na waziri wa zamani wa Serikali za awamu ya pili na tatu, Arcado Ntagazwa.
Chanzo-Mtanzania

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.