MSIMAMIZI WA UCHAGUZI BUNDA AKIRI KUKOSEA KUANDIKA IDADI YA WAPIGA KURA

Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika Jimbo la Bunda Mjini mwaka 2015, Lucy Msoffe amekiri kufanya makosa ya kuandika idadi ya wapigakura wakati wa kutangaza mshindi wa nafasi ya ubunge.

Akizungumza katika mahojiano na wakili wa upande wa mjibu maombi wa pili, Tundu Lissu katika kesi namba moja ya kupinga matokeo ya uchaguzi jimbo hilo inayoendelea mjini Musoma jana, msimamizi huyo alisema siku ya kutangaza matokeo alikuwa hajalala tangu tarehe 24 usiku hadi muda ambao alitangaza matokeo saa 11:11 jioni.

Alisema kutokana na uchovu mwingi ndiyo maana akawa anakosea kuandika idadi ya wapigakura mara mbili mfululizo wakati wa kutangaza mshindi. Sehemu ya mahojiano yao ilikuwa:

Lissu: Ieleze Mahakama kuwa wewe ulikuwa msimamizi wa uchaguzi wa majimbo matatu ya Wilaya ya Bunda, jimbo la Mwibara, Bunda na Bunda Mjini kweli si kweli.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli.

Lissu: Wewe ulikuwa msimamizi wa majimbo matatu ya uchaguzi katika wilaya hiyo kweli si kweli.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli.

Lissu: Ieleze Mahakama umeshika nafasi ya ukurugenzi kwa muda gani?

Shahidi: Nimekuwa mkurugenzi tangu mwaka 2007 na nimekuwa mkurugenzi katika sehemu mbalimbali hadi 2016.

Lissu: Ulikuwa msimamizi wa Uchaguzi Mkuu 2015 kwa mara ya pili kweli si kweli?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni sahihi.

Lissu: Ni kweli kwamba Jimbo la Bunda lilikuwa na vituo vya kupigia kura 467?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kumbukumbu yangu ninakumbuka kuwa idadi ya vituo ilikuwa 468.

Lissu: Ni kweli kabisa kuwa baadhi ya vituo hivyo viko visiwani?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli.

Lissu: Mweleze mheshimiwa Jaji siku ya tarehe 24/10/205 ulilala saa ngapi?

Shahidi :Mheshimiwa Jaji siku ya tarehe 24/10/2015 nililala saa nane au tisa hivi usiku.

Lissu: Tarehe 25/10/2015 uliamka saa ngapi?

Shahidi: Tarehe 25/10/2015 niliamka saa 11:30 alfajiri Lissu: Tarehe hiyo ulianza kupokea masanduku ya kupigia kura kuanzia saa ngapi?

Shahidi: Nilianza kupokea masanduku ya kupigia kura saa 11:30 jioni hadi tarehe 26/10/2015 saa saba mpaka nane usiku.

Lissu: Ni kweli zoezi la kuhesabu kura lilianza tarehe 26/10/2015 asubuhi?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, ndiyo zoezi lilianza saa 5:11 asubuhi.

Lissu: Ni kweli zoezi hilo lilienda hadi saa 11:11 jioni?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ndiyo.

Lissu: Kwenye fomu yako namba 24B ya kutangazia matokeo kuna namba 164,794 imefutwa futwa. Kweli si kweli?

Shahidi : Mheshimiwa Jaji ni kweli.

Lissu: Hiyo namba iko kweli idadi ya waliojiandikisha kwenye daftari?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli.

Lissu: Pembeni mwa namba hiyo iliyofutwa kuna namba 69,460 kweli si kweli?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli.

Lissu: Shahidi kielelezo P2 kina orodha ya vituo vya kupigia kura uliyowapatia vyama vya siasa kweli au si kweli?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli.

Lissu: Kielelezo hicho kilikuwa na idadi ya wapiga kura, kweli si kweli?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli.

Lissu: Mwishoni mwa hiyo karatasi uliyoshika kuna idadi ya wapigakura wa jimbo zima la Bunda Mjini wangapi?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji idadi ya wapigakura katika Jimbo la Bunda ni 69,369 .

Lissu: Idadi ya 164,794 ilikuwa ya kimakosa kweli si kweli?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kweli.

Lissu: Hizo tarakimu zilizokosewa za 164,794 ulizitoa wapi?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji nilizitoa kwenye idadi ya waliojiandikisha kwenye daftari kwenye majimbo matatu.

Lissu: Eleza idadi ya wapigakura kila jimbo.

Shahidi: Idadi ya kila jimbo ilikuwa kama ifuatavyo, Mwibara 59,436, Bunda Mjini 69,369 na Bunda ni 35,898.

Lissu: Jumla yake ni ngapi?

Shahidi: Jumla ni 164,794.

Lissu: Mbona hesabu yako ni tofauti na yangu? Hapa inaonyesha ni 164,703.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji labda nilikuwa nimekosea 

Lissu: Ilikuaje ukafuta 164,794 nini kilitokea?

Shahidi: Baada ya kujaza hii fomu na mawakala kusaini hii fomu nilienda kutangaza matokeo na wakati ninatangaza ndiyo wakaniambia kuwa nimekosea na nikafuta.

Lissu: Ulipofuta uliandika namba ngapi?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji niliandika 69,460.

Lissu: Hiyo namba mpya uliyoiandika ya 69,460 vilevile ulivikosea kweli si kweli.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli nilikosea.

Lissu: Sasa shahidi mueleze mheshimiwa jaji hayo makosa yaliyojitokeza mara mbili katika kujaza fomu yalitokana na nini?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji makosa hayo yaliyotokea mara mbili katika kujaza fomu yalitokana na uchovu niliokuwa nao.

Hadi tunakwenda mitamboni, kesi hiyo ilikuwa inaendelea.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.