
Lipuli FC imekuwa timu ya pili msimu huu (2017/2018) kuzivimbia Simba na Yanga kwenye uwanja wa Uhuru Dar katika mechi za ligi kuu Tanzania bara, baada ya leo November 26 kuibana na kuilazimisha Simba sare ya kufungana 1-1.
Kama unakumbuka, Yanga walijikuta wakilazimishwa sare ya kufungana 1-1 kwenye mchezo wao wa kwanza wa VPL msimu huu August 27, 2017 uliochezwa uwanja wa Uhuru. Lipuli walitangulia kufungana goli kupitia kwa ‘Karihe’ kabla ya Donald Ngoma kusawazisha badae.
Mtibwa Sugar ni timu nyingine ambayo imeweza kuchomoka bila kufungwa na vilabu vya Simba na Yanga kwenye uwanja wa Uhuru, Mtibwa waliikazia Yanga na kutoka suluhu October 1, 2017, huku Simba ikilazimisha sare katika dakika za majeruhi na kuambulia pointi moja October 15, 2017 pale timu hizo zilipotoka sare ya kufungana 1-1.
Simba inaongoza ligi baada ya kufikisha pointi 23 ikiwa imecheza mechi 11 hadi sasa, endapo kesho (Jumatatu November 28) Azam ikishinda dhidi ya Mtibwa Sugar itafikisha pointi 25 hivyo itaongoza ligi kwa kwa kuitoa Simba katika nafasi ya kwanza.
Sare ya Simba 1-1 Lipuli ni sare ya tano (5) kwa Simba msimu huu katika mechi 11 ambazo wameshacheza, hawajapoteza, wameshinda mechi sita (6).
Tags:
michezo